Tuesday, May 7, 2013

Na Joseph Ngilisho, Arusha
KAMA tulikuwa tunasubiri dalili kubwa zaidi zijitokeze ndipo tutambue kwamba hali ya nchi inatisha, tukio la bomu kutupwa kanisani, likasababisha vifo na majeruhi, lipimwe kama ishara ya juu kabisa.
Baadhi ya waumini wakiwa chini na wengine wakijaribu kujinusuru baada ya mlipuko wa bomu.
Pamoja na kila kinachosemwa kuzunguka tukio hilo, ukweli ni kwamba serikali ina kazi kubwa ya kufanya kutuliza mdudu hatari wa ubaguzi ambaye anaelekea kufanikiwa kuwagawa Watanzania kutokana na matukio ya aina hiyo.
Kudhihirisha hali ilivyo mbaya, maneno ya chuki ya kidini yalitawala jijini Arusha na katika mitandao ya kijamii kuzunguka nchi nzima, baadhi ya wakosoaji wakiwashutumu watu wa dini fulani kuhusika.
Baadhi ya majeruhi katika mlipuko huo.
NI UGAIDI TU
Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasit, Arusha, lililipuliwa na bomu la mkono, Jumapili iliyopita, saa 4:30 asubuhi.
Iliripotiwa juzi (Jumapili) kuwa mmoja wa watuhumiwa wa tukio hilo, anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, mtu huyo alikamatwa muda mfupi baada ya msako dhidi ya washukiwa kuanza.
Kuhusu chanzo au sababu ya wahusika kufanya ulipuaji huo, bado ni siri nzito lakini Watanzania wameshauriwa kuwa watulivu, kwani hilo ni moja ya matukio ya kigaidi ambayo yanapenyezwa nchini kwa sasa.
 Makamu wa Rais Dkt. Gharib Bilal, akimjulia hali mmoja kati ya wagonjwa waliokuwa mahututi aliyelazwa katika Hospitali ya Mount Meru.
“Sisi Watanzania tunajuana, hakuna Muislamu anayeweza kufanya shambulio dhidi ya Wakristo, kadhalika hakuna Mkristo anayeweza kufanya shambulio dhidi ya Waislamu, walipuaji ni magaidi, wakamatwe na washtakiwe kama magaidi.
“Haya maneno ya kusema watu wa dini moja wamewashambulia wa dini nyingine ni uchochezi mbaya na maneno ya aina hiyo yakiendelea yatatugawa Watanzania,” alisema Aminieli Moba, juzi, akiwa eneo la tukio, muda mfupi baada ya mlipuko.
Maneno ya Moba, hayapishani na ya Tito Hebrew, aliyeandika kwenye ukurasa wake wa Facebook: “Jamani hakuna udini, kuna chokochoko nyingi zinaibuliwa hapa. Watu walishataka kutugombanisha kwa njia za kisiasa wakashindwa.
“Kuna kipindi walijitahidi kutugombanisha kwa misingi ya ukabila ikawa ngumu, sasa hivi wanaamua kutumia njia za udini. Watanzania tunatakiwa tuutegue huu mtego, vinginevyo tutaingia kwenye vita ya sisi kwa sisi.”
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu, akitoa pole kwa mmoja wa majeruhi wa bomu juzi, katikati ni mwakilishi wa Papa hapa nchini, Askofu Francisco Padilla.
TUKIO LENYEWE
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, akiwemo mtoto mdogo (wote tunawahifadhi), mwanaume aliyevalia koti kubwa lenye kofia, akiwa amejifunika usoni, alitokea upande wa kushoto wa kanisa hilo kwa mbele na kutupa bomu hilo.
“Nilikuwa nimesimama ghorofani, nikamwona mtu akiwa na koti la mvua akisogea mbele ya kanisa na kurusha kitu kilichotoa mlio mkubwa na baadaye watu walianza kulia kwa sauti ndiyo nikajua lilikuwa ni bomu,” alisema shuhuda mmoja.
Shuhuda mwingine alisema: “Yule mlipuaji alikuwa na mwenzake na walifika pale kanisani wakiwa na gari. Baada ya kurusha bomu, alirudi kwenye gari kisha wakakimbia.”
Hata hivyo, shuhuda huyo ambaye ni mtoto mdogo, hakuweza kufafanua gari hilo ni aina gani wala namba zake za usajili.
Wanausalama wakiwa eneo la tukio.
VIFO
Kwa mujibu taarifa za vifo mpaka juzi jioni, watu watano walikuwa wamesharipotiwa kufariki dunia kutokana na tukio hilo.
Watu 42 walijeruhiwa katika shambulio hilo na wote walifikishwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru.
Waliojeruhiwa katika tukio hilo, wengi wao walionekana wakivuja damu nyingi, zilizolowanisha kabisa nguo zao.
Wengi wa waliojeruhiwa, walikatika viungo na wengine wamechanwachanwa, hivyo kuacha taharuki isiyomithilika.

MWAKILISHI WA PAPA CHUPUCHUPU
Mwakilishi wa Papa Francis I hapa nchini, Balozi Francisco Padilla, alinusurika kifo katika shambulio hilo.
Balozi Padilla aliyekuwa mgeni rasmi wa uzinduzi wa kanisa hilo, alikoswa na bomu, kwani lililipuliwa wakati akikamilisha ratiba za kubariki kanisa kabla ya kukata utepe, kuashiria mwanzo wa utoaji wa huduma za kikanisa.
Kanisa hilo ni jipya na ujenzi wake ulikamilika hivi karibuni, hivyo kugeuka gumzo kutokana, likitajwa kuwa moja ya makanisa yaliyojengwa kisasa kabisa ukanda wa Afrika Mashariki.
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu, pamoja na  mapadri zaidi ya 200, walihudhuria hafla hiyo ya uzinduzi wa kanisa hilo lakini wote wamenusurika.
NI MAAFA KATIKATI YA SHEREHE
Msemaji wa Kanisa Katoliki Parokia ya Olasit, Father Festus Mwangwangi, alisema kuwa sherehe za uzinduzi zilianza vizuri lakini mambo yaliharibika baadaye.
Alisema, kabla ya tukio hilo waumini wa kanisa hilo walianza maandamano kuanzia Kanisa Katoliki la Burka ambalo ni kanisa mama, wakiongozwa na Askofu Lebulu, na ilipofika saa 3.30 asubuhi, walifika katika kanisa hilo la Mtakatifu Joseph.
“Maandamano yalipokamilika, balozi wa Vatican (mwakilishi wa Papa), aliwasili katika msafara wake na mwenyeji wake ambaye ni Askofu Lebulu, kisha akamtembeza kulikagua kanisa hilo.
“Baada ya kulikagua kanisa, lilifuata tendo la kubariki maji ambayo yangechanganywa na chumvi kisha kutumika kulibariki kanisa lakini tukiwa kwenye hatua ya kubariki maji ndipo mlipuko mkubwa ulisikika,” alisema Father Mwangwangi.

UVUMI KUHUSU SIASA
Kwa upande mwingine, yapo madai yaliyopo mkoani Arusha kwamba bomu hilo pengine ni njama za wanasiasa.
Inadaiwa kuwa kuelekea uzinduzi wa kanisa hilo, kuna mmoja wa mawaziri wakuu wastaafu, alitajwa sana kuwa angekuwa mgeni rasmi.
“Pengine watu wabaya dhidi ya huyo mheshimiwa, waliamini huo uvumi, sasa wakaona hiyo ndiyo sehemu ya kutekeleza njama zao,” alisema mkazi mmoja wa Arusha, Philipo Abdiel.

LEMA AKOSOLEWA
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, alifika eneo la tukio muda mfupi baada ya bomu kulipuka na kutoa matamshi makali dhidi ya serikali na udini.
Hata hivyo, wananchi wa Arusha waliozungumza na Uwazi, walisema kuwa wanamheshimu sana Lema na wanampenda kama mbunge wao lakini anakosea kuweka siasa katika tukio zito kama hilo la ugaidi.
“Kuna mambo akichanganya na siasa itakuwa sawa lakini siyo hili. Lema anatakiwa kushirikiana na serikali katika vita dhidi ya ugaidi ambao unapenyezwa nchini,” alisema Rosemina Kiwia, mkazi wa Ngarenaro, Arusha.

POLISI WANENA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema: “Uchunguzi makini utafanyika. Hapa tutawaleta wataalamu wa mabomu na baada ya uchunguzi ndipo tutatoa taarifa rasmi ya jeshi la polisi.”

MKUU WA MKOA
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, aliwataka wananchi kuwa watulivu wakati vyombo vya dola vikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
“Polisi kutoka makao makuu ya jeshi pamoja na wataalamu wa mabomu kutoka makao makuu wanatarajiwa kufika katika eneo la tukio ili kuongeza nguvu,” alisema Mulongo.

No comments: