Tuesday, December 15, 2009


Mkurugenzi wa Msama Promotions,Alex msama akizungumza na mchungaji
Mama Getrude Lwakatare kwenye moja ya tamasha la Msama Promotions hivi karibuni

KAMPUNI ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam, imeandaa tamasha la kimataifa la nyimbo za injili, litakalofanyika Desemba 25, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi, Alex Msama,amesema kuwa tamasha hilo ni tamasha litakalowaunganisha waimbaji kutoka nchi za Kenya, Malawi, Uganda, Burundi Zambia na Afrika Kusini. Alisema, lengo la tamasha hilo ni kusaidia watu wenye ulemavu na yatima na wengine wenye mahitaji ambao wanapaswa kusaidiwa katika jamii.

“Ujue kuna baadhi ya watu wenye ulemavu ambao wanahitaji misaada mbalimbali, kwa mfano baiskeli, hivyo kampuni yangu imeliona hilo, hivyo tumepanga kuelekeza nguvu kwa walemavu wa mikoani,” alisema Msama na kuongeza. Fikiria kuna wengine wanatamani kusoma, lakini kwa kukosa usafiri na huduma nyingine muhimu, wanashindwa, hivyo tumeona ni vizuri kama tutawakumbuka,” alisema Msama.

Msama aliyechangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa muziki wa injili akiwa mwasisi wa matamasha ya injili, alisema katika tamasha hilo, pia kutakuwa na waimbaji wapya walioingia katika albamu ya Haleluya Collections Volume 5, wakiwamo kutoka Tanzania. Msama alisema kamati hiyo imeamua kufanya matamasha mara mbili kwa mwaka ikiwa ni kufanyia kazi maoni ya wapenzi na mashabiki wa muziki huo.

Kuhusu misaada kwa makundi mbalimbali ya kijamii, Msama alisema kamati yake imekuwa ikifanya hivyo ikiwa ni sehemu ya wajibu wa kusaidia wenye mahitaji katika jamii. Alisema, kamati hiyo imekuwa ikimuomba Mungu azidi kuijalia uwezo kwani lengo ni kugawa baiskeli 100 kila mwaka badala ya 70, ilizowahi kugawa na kusomesha yatima. Mbali ya baiskeli, kamati hiyo imewahi kutoa vitanda vya wagonjwa katika hospitali mbalimbali nchini ingawa kwa kipindi hicho hawakuwa wakitangaza hadi pale waliposhauriwa kufanya hivyo.

Alisema kuanzia sasa, watakuwa wakitangaza hata mapato katika matamasha mbalimbali ili kuwa wazi zaidi, kwani hiyo pia itawajengea imani zaidi kwa jamii. Aidha, Msama ametoa wito kwa watu mbalimbali katika jamii kuguswa na suala hilo, kwani linalenga kusaidia makundi maalumu katika jamii. Sambamba na hilo, Msama ametoa wito pia kwa jamii kuunga mkono juhudi za kamati hiyo kwa kununua albamu ya Haleluya Volume 5 iliyoko madukani.

No comments: