Mwalimu afundisha shule nzima yeye peke yake! Duh!
Mkuu wa Sekondari Kibungo Juu, Tarafa ya Matombo, Bw. Chapembe Chapembe, ndiye mwalimu pekee anayefundisha wanafunzi 270 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne na amelazimika kutoifunga shule hiyo kwa likizo iliyoanza Juni mwaka huu.
Uamuzi wa kuendelea kufundisha madenti hao wakati wa likizo ni kwa ajili ya kuwawezesha madenti wa kidato cha nne na pili ambao wanatarajia kufanya mitihani yao mwaka huu wamudu vyema kufaulu masomo yao.
Mwalimu Mkuu huyo alisema hayo juzi mjini Morogoro katika hafla ya kumkabidhi pikipiki kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mh. Issa Machibya, baada ya kutambua ushupavu wake wa kujituma katika kufundisha kwenye mazingira magumu, uwajibikaji na kuipenda kazi yake.
Kwa mujibu wa Mwl. Chapembe, shule hiyo ilianza mwaka 2007, na kati ya wanafunzi hao 114, wasichana ni 81, mwaka huu ilipangiwa wanafunzi 79 wa kidato cha kwanza na inatarajia kutoa wanafunzi zaidi ya 53 wa kwanza wa kidato cha nne.
Alisema shule hiyo iliyopo katika uwanda wa milima na miinuko, inakabiliwa na changamoto za kukosa walimu na nyumba za kuishi, hali iliyomfanya kubaki peke yake na mwaka huu wanafunzi wake watafanya mitihani ya kumaliza sekondari.
“Walimu wote wanaopangiwa Kibungo Juu hufika na kuondoka kutokana na mazingira magumu … usafiri ni wa shida na nyumba hakuna,“ alisema Mkuu wa Shule.
Aliongeza: “Mimi mwenyewe ninaishi Kijiji cha Kiswira ni umbali wa zaidi ya kilometa 40 kutoka ilipo shule, na mara nyingi nalazimika kupiga kambi shuleni ili kuwafundisha vizuri wanafunzi wangu,” alisema.
Mkuu huyo alisema amelazimika kuwatumia wanafunzi wa kidato cha nne wa Sekondari ya Tawa kufundisha wenzao wanaotarajia kufanya mitihani mwaka huu kwa baadhi ya masomo.
Wanafunzi wa shule hiyo wengi wao wana uwezo mkubwa kiakili, lakini wanachokosa ni nyongeza ya maarifa na mbinu za kitaaluma kutoka kwa walimu wenye taaluma ya masomo ya sekondari.
“Bado ninawahurumia wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne kama watamudu kufanya mtihani kikamilifu … ninaona ipo hatari ya wanafunzi kushindwa mitihani yao ya mwaka huu,” alisema Chapembe.
No comments:
Post a Comment