Wednesday, June 16, 2010

Sakata la "Kikwete" na "Mimba za Vihelehele" laombewa msamaha


Shikamoni watanzania wote. Watoto msisite kuitikia salamu yangu ambayo ndani yake ina unafiki wa kuonesha jinsi gani nilivyomuungwana kwa watu wote.
Moyoni nataka kutimiza lengo langu la kisiasa la kumuombea msamaha Rais wangu Jakaya Kikwete kuhusu kauli aliyoitoa Kijijini Kisesa wilayani Magu mkoani Mwanza, kwamba kukithiri kwa mimba mashuleni kunachochewa na viherehere vya wanafunzi wenyewe.

Kwa haki ya Mungu aliye juu, nachukua nafasi hii, kumuombea radhi kwa Watanzania wote Rais Kikwete kwa sababu ni mmoja kati ya ndugu zangu, yaani nimekuwa rafiki wa familia ya marehemu dada yake aliyekuwa anakaa mtaa wa Mtoni pale Temeke, jirani na eneo la Sokota, nazungumzia jijini Dar es Salaam.
Mkiniona chozi langu namaanisha nina tikiswa kumtima na haka ka kauli ka ndugu yangu, ambako kamewafanya Wanyamwezi wenzangu, licha ya vitabia vyao vya kupenda ‘totozi’ wakutane kimila kujadili kama ni kweli watoto wao wanabeba mimba kwa viherehere vyao au ni hali isiyovumilika inawaondolea uvumilivu watoto na kujikuta watake wasitake wanalazimika kufanya ngono.

Mzee Maganga, kikao chenu kina maana sana na ni kweli mtakuwa mmekasirika, lakini mnashindwa kufahamu kuwa kama ninyi msivyobahatika kuingia Ikulu, na Rais naye hajapata bahati ya kujionea maisha ya watoto wenu na shida mnazokutana nazo.
Aliposema hivyo alikuwa hajui kama watoto wenu wa kike wanakata misitu minene kabla ya kuifikia shule yenu ya sekondari ya kata mliyojenga kwa lazima ya yule kiongozi shujaa aliyeng’atuka kwa kale ka tuhuma ka umeme.
Kati yenu ni nani aliyemwambia Rais Kikwete kwamba kuna baadhi ya wanafunzi mmewapangisha kwenye nyumba za nyasi zilizopo kijiji jirani na shule na kwamba huko wanajihudumia kwa kila kitu?

Mlimwambia Rais kwamba ninyi wazazi hamna uwezo wa kuwapatia hata thumni ya chumvi watoto wenu kwa vile mmekatazwa kuuza mazao yenu nje ya nchi na tena mmekopwa mazao na vyama vya ushirika ambavyo vinatarajia kuwalipa kidogo kidogo mwishoni mwa mwaka huu?
Unaona sasa! Wote mnatikisa vichwa kuonesha hamjamwambia! Hii ina maana kwamba rais hajui maisha yenu, yeye kazoea kuwaona watoto wa mjini wakienda shule kwa magari na shilingi mia mbili mfukoni. Kwa mazingira hayo atakuwa na kosa kweli kutamka kuwa watoto wenu wanaviherehere vya mabwana? Aaa, jamani mbona mnataka kumfanyia tambiko kwa kumuonea mtoto wa mwenzenu, kumbukeni ni mtani wenu huyo!

Kama nilivyosema mwanzo, naandika uchochezi huu kumuombea radhi mkuu wangu, nikikiri kwamba kidogo sana, narudia tena, kidogo alikosea kusema hivyo na kilichomkosesha baada ya mimi kumsoma nilipokuwa naye kichwani kwa uchambuzi wa suala hili la mimba kwa wanafunzi ni kudanganywa na wasaidizi wake.
Kinachotokea siku hizi, wengi wao wanaogopa kutimuliwa kazi, hivyo huwa hawataki kueleza ukweli, mtakumbuka hata janga la njaa lilipotokea kijijini kwenu mkuu wenu wa wilaya alidiriki kusema kwamba hamna njaa na kwamba stoo zenu zilikuwa na chakula cha kutosha.

Sasa tusikimbilie huko nafahamu kwamba walikufa akina Mataluma, Mwana Ushi na watoto wa mzee Mikidadi wawili katika njaa hiyo, huo ulikuwa ni mfano tu wa namna viongozi wa juu wanavyoweza kutoa taarifa za uongo kwa lengo la kulinda posho zao. Msibubujikwe na machozi wazee, Rais hakuwa na nia ya kuwakejeli watoto wenu alikosea kutokana na ‘data’ ndiyo maana alisahau hata kama kondomu hazifiki kwenu na kwamba hata zikifika hamna uwezo wa kununua.

Mzee Kapaga bado hamjanielewa? Nadhani sasa naanza kuona mkono wa kisiasa ndani ya kauli hii, maana kama ni kosa la mimba za viherehere mbona nimeshalifafanua sana, au mnataka niwageukie na ninyi kuhusu uharibifu wa mila mlioufanya mpaka watoto wenu wamekuwa hawaheshimu usichana wao.
Hata kama utandawazi umeharibu tabia za watoto wenu ni jukumu lenu kama wazazi kuwakataza wanenu waache

No comments: