
Imefahamika kuwa majambazi mawili yaliyouawa na polisi mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Arusha saa 5.40 asubuhi katika eneo la Unga LTD walikuwa wakivizia kupora fedha zinazodaiwa kuwa ni mishahara iliyokuwa ikitolewa benki.
Akielezea tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Basilio Matei alisema kuwa jeshi la polisi lilipata taarifa za siri kuwa majambazi hao walipanga kupora mishahara ambayo hata hivyo hakuweka wazi ilikuwa ikipelekwa kwenye kampuni ipi.
Alisema kuwa jeshi hilo liliandaa mpango wa siri na kugundua gari walilokodisha ambalo ni Toyota Corolla na kuwafuata nyuma kwa gari binafsi na walipofika katika Barabara iendayo eneo la Faya majambazi hao waligundua kuwa wanafuatiliwa.
“Mara baada ya kubaini kuwa wanaowafuatilia ni askari walijihami kwakufyatua risasi hewani na ndipo polisi walipojibu shambulizi hilo na kuwafyatulia risasi ambapo wawili waliuawa,” alisema Kamanda Matei.
Kamanda Matei aliwataja waliouawa kuwa ni Erick Massawe (35), Mkazi wa Kijenge na Michael Raphael (36), Mkazi wa eneo la Sanawari na kwamba jeshi hilo bado linamtafuta mmoja aliyekimbia .
Utata unajitokeza kuhusu mauaji hayo kwani inadaiwa majambazi hao waliuawa wakiwa ndani ya gari ambalo linahusishwa na jeshi la polisi na kuwepo kwa tundu moja ya risasi ambalo linaonekana ni risasi iliyongia ndani ya gari na siyo kutoka.
Pia dereva wa gari walilokuwepo watu hao waliotajwa kuwa ni majambazi hafahamiki alipo na wajihi wake .
Wananchi walioshuhudia tukio hilo wamedai kuwa, hakukuwa na majibishano ya risasi kati ya polisi na majambazi hayo.
“Jeshi la polisi linahitaji kujipanga zaidi na pengine hata kujisafisha kufuatia baadhi ya askari wake kuhusishwa na uhalifu wa kushiriki ujambazi,” alisema mwananchi mmoja aliyeomba jina lake kuhifadhiwa.
Matei pia amebainisha kuwa polisi jijini Dar es Salaam inawashikilia majambazi wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya mfanyabiashara wa Kiarabu, Salehe Hussen Ally ,ambapo mbali na mauaji, yalifanikiwa kupora mamilioni ya shilingi katika duka la la Burj Al Arab lililopo katikati ya mji wa Arusha. Majambazi hayo yataletwa jijini Arusha.
No comments:
Post a Comment