Wednesday, June 16, 2010

Majambazi watetemesha Arusha!!

Na Woinde Shizza
wa Michuzi Blog (Globu ya Jamii), Arusha

Kundi la majambazi watatu wakiwa na silaha nzito limeua watu wawili akiwemo mfanyabiashara mwenye asili kiasia na kupora mamilioni ya fedha mijni hapa.

Tukio hilo ambalo limethibitishwa na polisi mkoani hapa limetokea jana majira ya saa kumi na nusu jioni katika mtaa wenye shughuli nyingi za kibiashara wa Sonali Soko Kuu mjini Arusha.

Watu walioshuhudia tukio hilo wamesema kuwa kabla ya mauaji hayo majambazi, ambayo idadi yake yake kamili haijaweza kufahamika, yaliteka mtaa huo na kupiga risasi hovyo hewani na kusababisha taharuki katika eneo hilo na maeneo ya jirani.

Katika tukio hilo mfanyabiashara Swaleh Hussein Alli (35) aliuawa kwa kupigwa riasi kadhaa kichwani na kufariki dunia papo hapo, huku mfanyabiashara ndogo ndogo mwanamama Paschalina Antony (32) mkazi wa Unga Limited aliuawa kwa kupigwa risasi kifuani wakati akipiga mayowe bada ya kushuhudia majambazi hayo yakammiminia risasi Alli.

Mashuhuda hao walisema kuwa kabla ya tukio hilo walifika watu kadhaa na kuingia katika duka la mfanyabiashara huyo wakijifanya wanataka kufanya manunuzi. Ghafla tu watu hao kila mmoja akiwa na silaha walimnyooshea bunduki mfanyabaishara huyo na kuwaamuru wafanyakazi wa duka hilo kulala chini na kuanza kumiminia risasi mfanyabaishara huyo.

“Tukio lenyewe lilikuwa kama filamu hivi watu hao waliingia dukani kama wateja wakauliza bei ya nguo na vitu vingine wakati tunajaribu kuwaonyesha ghafla wakageuka na kukaa kila upande na silaha wakatuamuru kulala,tulichiosikia ni milio ya risasi na harufu ya damu tulipoamka tukamkuta tajiri yetu amekufa”alisema mmoja wa watumishi wa duka hilo ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini.

Naye John Kumbau mfanyabiashara wa soko kuu alisema kuwa majambazi hayo yalikuwa mengi na yalipofika katika eneo hilo yalijigawa katika makundi matatu na kuhakikisha kuwa hayana mtu wa kuwazuia baada ya tukio.

“Unajua mimi niliona kila kitu kwa hofu ya kuuawa nikanyamaza kimya,yule mama aliyeawa alipiga kelele nikaona akipigwa nikakaa kimya lilikuwa tukio la kutisha”alisema Kumbau

Akizungumzia tukio hilo kamanda wa jeshi la polisi mkoani hapa Basilo Matei alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa majambazi hayo yalikuwa na gari aina Toyota Corrola Premio lenye rangi ya kijivu ambapo mapaka sasa namba zake za usajili hazijaweza kufahamika.

Kamanda Matei alibainisha kuwa uchunguzi wa awali unaoonyesha gari hilo liliporwa kutoka mjini Moshi siku tatu kabala ya tukio hilo .

“Baada ya tukio hilo tulifanya mawasilianio ya haraka na majirani zetu ,tukajulishwa kuwa gari hilo lililotumika liliporwa kutoka Kilimanjaro”alisema Matei.

Aidha aliwataka wananchi mkoani hapa kutoa taarifa zozote zitakazoasaidia kukamatwa kwa wahusika wa tukio hilo baya kuwahi kutokea katika siku za hivi karibuni.

“Wahusika wa tukio hili lazima watakamatwa hawataweza kuuushinda mkono mrefu wa dola kila mahali tumejizatiti ni lazima watiwe nguvuni.

Tukio hilo kubwa la mauaji na uporaji ndilo tukio kubwa kuwahi kutokea mwaka huu baada ya watu wanaoasadikiwa majambazi kumwua mwanamke mmoja aliyetajwa kwa jina Jackline Deo mkazi wa Lemara mwishoni mwa mawezi januari mwaka huu ambapo hata hivyo katika tukio hilo majambazi hayo hayakuchukua kitu chochote na baada ya siku tatu nao waliuawa na polisi.

No comments: