Tuesday, September 7, 2010

Dr. Slaa afunguliwa Mashataka

MGOMBEA urais kwa tiketi ya CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa (pichani), amefunguliwa kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaami, akidaiwa fidia y ash. bilioni moja kwa madai ya kunyang’anya mke wa mtu.

Kesi hiyo namba 122 ya mwaka 2010, ilifunguliwa leo mahakamani hapo na Aminiel Mahimbo kwa kupitia ofisi ya mawakili ya Amicus.

Mahimbo anadai kuwa, Dk. Slaa kamnyang’anya mkewe wa ndoa Josephine Mushumbusi.

Kwa kupitia nakala ya hati ya madai, Mahimbo anadai fidia ya sh. milioni 200 kutokana na hasara alizozipata baada ya mdaiwa huyo, kumtangaza mkewe wa ndoa Josephine kuwa mchumba wake na sh. milioni 800 ikiwa ni hasara ya jumla aliyopata.

Mlalamikaji huyo, anadai Septemba 7, 2002 alifunga ndoa na mwanamke huyo katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ushirika wa Kijitonyama na kuishi maeneo mbalimbali ikiwemo Kimara, Baruti, Dar es Salaam.

Pia anadai katika maisha yao ya ndoa wamebahatika kuwa na watoto wawili ambao ni Upendo aliyezaliwa Mei Mosi, 2003 na Precious aliyezaliwa Machi 14, 2007.

Mahimbo alidai, ndoa kati yake na Josephine haijavunjwa na chombo chochote na kwamba, bado ni mke wake halali.

Kwa mujibu wa hati hiyo, Mahimbo alidai hivi karibuni, mkewe alikuwa na safari za mara kwa mara na aliamini ni za kikazi. Josephine ni mfanyabiashara ambaye anaendesha kampuni iitwayo Green World Clinic.

Alidai katika tarehe na mahali tofauti, Dk. Slaa alimtambulisha mwanamke huyo kuwa ni mkewe, suala ambalo si kweli.

Mlalamikaji huyo alidai, uhusiano uliopo kati ya watu hao wawili umemfanya adhalilike na kunyanyasika katika jamii na anaiomba mahakama kumzuia Dk. Slaa kuendelea kujihusisha kimahusiano na mkewe.

Anaiomba mahakama kumwamuru Dk. Slaa kumlipa bilioni moja na kulipa gharama za kuendeshea kesi.

Mahimbo amedai ameambatanisha na cheti cha ndoa na Josephine, picha za harusi, vyeti vya kuzaliwa vya watoto na nakala za vipande vya magazeti zilizopigwa wakati Dk. Slaa akimtambulisha mwanamke huyo kuwa ni mkewe.

No comments: