This blog is for critical thinkers, people with open mind, ready to accept criticisms and work on them. Sharing the know-how, skills and experiences of Life and Technology at large. You are warmly welcome!! ---------------------------------------------------- Blogu hii ni kwa ajili ya wenye fikra makini wapendao kupokea na kufanyia kazi ukosoaji. Walio na mtazamo chanya tena mpana katika kushirikishana maarifa, ujuzi na uzoefu wa maisha na teknolojia kwa ujumla wake. Karibuni sana !!!
Tuesday, September 7, 2010
Mume aeleza alivyoporwa mke na Dk. Slaa
Aminiel Mahimbo Mume wa ndoa wa Josephine Mushumbusi
NAKUACHIA kibanda chako, nakwenda kwenye nyumba yangu.”
Hayo yalikuwa maneno ya mwisho ambayo Aminiel Mahimbo aliambiwa na mkewe, Josephine Mushumbusi siku alipoachwa na mkewe huyo aliyeamua kwenda kwa mgombea wa urais wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa.
Mahimbo ambaye ni mume halali wa Josephine, (kwa ndoa ya kanisani) alisema anakumbuka kuwa ilikuwa Machi mwaka huu na hakujua mke wake alipokuwa akienda na wala hakuhisi dalili yoyote ya kuwepo kwa mwanamume mwingine katika ndoa yao mpaka siku mwanawe wa kwanza Upendo (7) alipomwambia “baba tunaishi na daddy”.
Akisimulia kisa hicho kilichoanza takribani miezi saba iliyopita, katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana, Mahimbo ambaye ndoa yake ilifungwa Agosti 16, 2002 na Mchungaji Lewis Hiza katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Kijitonyama, jijini Dar es Salaam, alisema hakujua kama huyo ‘daddy’, ni Dk. Slaa mpaka siku moja alipoambiwa na mama mkwe wake.
“Baada ya (Josephine) kuondoka nyumbani, tulikwenda mpaka nyumbani kwao kusuluhishana, lakini alikataa katakata kurudi nyumbani na wazazi walikasirika na kumfukuza.
“Siku moja mama mkwe alikuja Dar es Salaam (kutoka nyumbani kwao Mwanza) na alikwenda kumtembelea mama yangu Kijitonyama,” alisimulia.
Alisema alipopata taarifa ya kuwepo kwa mama mkwe wake Dar es Salaam, aliwasiliana naye kwa simu na katika mazungumzo hayo mama huyo alikuwa akilia huku akimwambia kuwa mume mpya ni Dk. Slaa.
“Nilimpigia baba yake mdogo, Ruhendela (hafahamu jina la pili anahisi ni Mushumbusi ambalo ni la ukoo) kutaka kufahamu ukweli wenyewe, akathibitisha hilo na kusisitiza kuwa familia haimtambui mheshimiwa, inanitambua mimi,” alisema.
Kabla ya kufahamu hilo, Mahimbo alisema siku moja ilikuwa sikukuu, akaomba kupewa watoto awapeleke kwa bibi yao, na walipokuwa njiani, mwanawe Upendo alimwonesha hoteli ambayo Josephine, Dk. Slaa na watoto hao walikuwa wakiishi.
“Sikumbuki jina, ila ipo barabarani ukishapita Makongo maeneo ya Tegeta na siku hiyo baada ya kuwarudisha watoto, mama yao aligundua Upendo katoa siri ya mahali wanapoishi.
“Alimpiga na baada ya hapo akanipigia simu na kumpa Upendo aongee na mimi, alikuwa akilia akisema baba njoo unichukue siwezi kuishi huku,” alisimulia Mahimbo.
Alisema wakati akijitayarisha kwenda kumchukua mwanawe, ndugu zake walimshauri asiende kwa kuwa ilikuwa saa tatu usiku na walikuwa wakihofia usalama wake.
Kwa mujibu wa Mahimbo, mama mkwe wake alimwambia kuwa Dk. Slaa na Josephine, walihamia katika hoteli ya Abla Hotels Apartment iliyopo Victoria Dar es Salaam.
“Nafikiri bado wapo hapo, juzi juzi nilikwenda hapo kutaka kuonana na mheshimiwa (Dk. Slaa), waliniambia kuwa yupo ndani amepumzika siwezi kumuona muda huo,” alisema Mahimbo.
Gazeti hili liliwasiliana na hoteli hiyo kwa simu ambapo mhudumu mmoja alisema hawezi kuelezea taarifa za watu, lakini akathibitisha kuwa Dk. Slaa alikuwa akiishi hapo.
Mahimbo alisema aliwasiliana na Mchungaji Hiza ambaye aliahidi kuzungumza nao tofauti kabla ya kuwaita pamoja kwa ajili ya usuluhishi.
“Nimeongea na Mchungaji Hiza, amesema ameshazungumza na Josephine na ataniita kwenda kuzungumzia hilo, juzi alikuwa Dodoma kulikuwa na mkutano wa viongozi wa dini,” alisema.
Pia Askofu Mkuu wa KKKT, Alex Malasusa alipohojiwa alisisitiza kuwa hawezi kuzungumzia hilo kwenye simu.
Hata hivyo Mahimbo alisema zamani alikuwa akizungumza na watoto wake, Upendo na Precious, lakini kwa sasa ana miezi miwili au zaidi ya mmoja tangu awaone watoto hao na hata simu siku hizi hawapewi.
Mahimbo alisema hakuwahi kuhisi kwamba mkewe alikuwa akiisaliti ndoa yao na mara kwa mara alikuwa akisafiri kwenda mikoani hasa Dodoma wakati wa Bunge akijua ni kikazi mpaka alipofahamu kuwa mkewe anaishi na Dk. Slaa, ndio aliposhituka kuwa safari za mkewe Dodoma hazikuwa za kikazi tu.
Alisema mpaka sasa Josephine ni mke wake halali, lakini hana hakika kama wanaweza kurudiana tena kwa kuwa amemdhalilisha.
Na wakati Mahimbo akiwa njia panda akishindwa kujua hatima ya ndoa yake, Dk. Slaa, Padri msomi `amelitangazia’ taifa mbele ya mikutano ya kampeni ya chama chake cha Chadema kuwa Josephine ndiye mke wake mtarajiwa.
Katika kudhihirisha kuwa `hatanii’, amekuwa akizunguka naye katika mikoa mbalimbali nchini anakopita kufanya kampeni ya kuomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania baadaye mwaka huu.
Dk. Slaa alidiriki pia kumkana mke wake wa miaka nenda miaka rudi, Rose Kamili aliyezaa naye watoto wawili, akidai kwa sasa hana mahusiano naye, bali ana `chombo kipya’, Josephine.
Ni baada ya kumtangaza Josephine ndipo habari zilipovuja kuwa, mwanamke huyo anayetamba naye Dk. Slaa ni mke wa mtu aliyefunga ndoa kanisani mwaka 2002, lakini akaamua kuondoka katika mazingira ya kutatanisha na kutua kwa mgombea huyo wa urais kwa tiketi ya Chadema.
Kwa upande wa Rose, mwanaharakati na mwanasiasa aliyeiongoza CCM katika Kata ya Basotu Hanang akiwa Diwani kwa miaka 16 kabla ya kuhamia Chadema hivi karibuni na kutangaza kugombea ubunge Hanang, amekuwa kimya kuzungumzia suala la mumewe.
Na hata juzi walipokutana katika kampeni za Dk. Slaa mkoani Manyara.
Rose ingawa alikuwa jukwaa moja na Josephine alionesha ukomavu kwa kujali kampeni zake hadi mgombea huyo wa urais alipoondoka Hanang kwenda Mbulu kuendelea na kampeni zake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment