Wednesday, September 15, 2010

Kumbe Kikwete analindwa na Majini!


Na Elvan Stambuli
MNAJIMU maarufu Afrika Mashariki, Sheikh Yahya Hussein, amesema katika taarifa yake ya Septemba 9, mwaka huu aliyozungumzia kumpa ulinzi usioonekana Rais Jakaya Mrisho Kikwete hakuzungumzia nguvu za giza au uchawi na badala yake alizungumzia ulinzi wa majini ambayo yapo duniani kote.

Akizungumza na mwandishi wetu nyumbani kwake jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Sheikh Yahya alisema, “ Mimi sikuzungumzia nguvu za giza na wala sifanyi uchawi au ushirikina nilikuwa nazungumzia Majini ambao ni viumbe kama sisi, isipokuwa wao wameumbwa kwa moto na sisi tumeumbwa kwa udongo na wametajwa katika vitabu vyote vitakatifu vya Waisalamu na Wakristo na Mwenyezi Mungu amesema tushirikiane nao.”

Akifafanua zaidi mnajimu huyo alisema kila binadamu ana jini na akatoa mfano wa Mfalme Solomon ambaye anatajwa katika vitabu vitakatifu vya kidini alikuwa na Jeshi la Majini na aliwatumia katika ujenzi na vita na hata Rais wa nne wa Indonesia marehemu Abdulrahman Wahid aliyetawala kati ya mwaka 1999 mpaka mwaka 2001 aliwatumia sana Majini kwa ulinzi wake binafsi na mikutano ya chama chake kiitwacho National Awakening Party ( PKB).

“Kwa hiyo nawataka viongozi wa kidini na kisiasa wasihusishe mambo haya na uchawi, haya ni mambo ya kawaida na yanafanyika ulimwenguni kote hata hao viongozi wa kidini nao wanawatumia Majini katika kazi zao, na viumbe hivi vipo anayebisha asome vizuri vitabu vya dini na kamwe siyo uchawi,” alisisitiza mnajimu huyo.

Hivi karibuni Sheikh Yahya alisema atamuongezea ulinzi usioonekana Kikwete, kauli ambayo ilitafsiriwa na baadhi ya wanasiasa na viongozi wa dini kuwa ni mambo ya kichawi na nguvu za giza, hivyo kumshutumu.

No comments: