By BBC
Waziri wa uhamiaji atasema, idadi ya wanafunzi wa kigeni wanaoruhusiwa kuingia Uingereza "haikubaliki."
Katika hotuba itakayotolewa baadae, atahoji iwapo Uingereza inawavutia wanafunzi bora- ikiwa nusu tu ya visa zinazotolewa kwa wanafunzi zimetolewa kwa wale wanaosomea elimu ya juu.
Kauli za Bw Green zinatolewa huku utafiti wa wizara ya mambo ya ndani zikisema moja ya tano ya wanafunzi bado wako Uingereza, miaka mitano baada ya kupewa viza.
Wizara hiyo imewafanyia utafiti wahamiaji ambao hawatoki Ulaya waliokuja Uingereza mwaka 2004.
Kundi kubwa zaidi- takriban watu 185,000- walikuwa wanafunzi, na asilimia 21 bado walibaki nchini hata miaka mitano baadae.
Mwandishi wa BBC wa masuala ya mambo ya ndani Danny Shaw alisema, pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wa kigeni, Bw Green ameamua suala la mabadiliko ya uhamiaji wa wanafunzi kulipa kipaumbele
'Shagalabagala'
Mawaziri pia wana nia ya kutathmini viza za kufanyia kazi kwani mbili ya tano ya kundi hilo wamebaki Uingereza baada ya miaka mitano.
Kabla ya hotuba yake, Bw Green alisema: " Hatuwezi kuhisi tu kuwa kila anayekuja hapa ana uwezo ambao Uingereza hauna."
Aliiambia kipindi cha redio cha BBC Radio 4: " Sitaki kuingilia mafanikio yaliyopatikana kwenye vyuo vyetu."
Bw Green alisema: "Kwanini wanabaki? Wanabaki kufanya nini? Hili ni jambo tunalotakiwa kuliangalia kwa upana zaidi hasa katika mfumo wa uhamiaji."
Ofisi ya takwimu za taifa zilizotolewa mwezi uliopita zilionyesha uhamiaji umeongezeka kutoka 33,000 hadi 196,000 kwa mwaka 2009.
Idadi ya viza zilizotolewa kwa wanafunzi zimeongezeka kwa asilimia 35 hadi kufikia 362,015.
Bw Green alisema takwimu hizo ni ushahidi tosha kuwa serikali ya muungano ilirithi mfumo wa uhamiaji ambao uko "shagalabagala"
Alisema, " Takwimu hizo zinaniambia kwamba tunatakiwa kuangalia njia nyingine zote zinazotumiwa na watu kuingia nchini, labda kwasababu ya elimu, sababu za kuungana na familia, na pia, hasa, njia zinazowapa ukaazi wa kudumu."
No comments:
Post a Comment