Tuesday, September 7, 2010

Mwanamke abakwa hadi kufa Arusha!

MWANAMKE mmoja mkazi wa Kitongoji cha Kisambare, Usa River wilayani Arumeru, amebakwa hadi kufa na kundi la wanaume akiwemo mumewe wa ndoa.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Basilio Matei (Pichani chini)amemtaja marehemu huyo kuwa ni Juliana Zacharia (38) na mumewe Stewart Yesaya Msemo anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kula njama na wabakaji kufanya kitendo hicho.

Kamanda Matei alisema kuwa tukio hilo la kusikitisha lilitokea majira ya usiku katika nyumba ambayo bado inajengwa baada ya kuburuzwa kutoka eneo alilokuwepo na kuingiliwa kwa zamu na wanaume hao.

Alisema kuwa kabla ya tukio hilo, marehemu alikuwa na ugomvi na mumewe uliosababisha watengane kwa muda na kwamba siku ya tukio Juliana alionekana katika baa moja akiwa na mumewe huyo wakinywa pombe huku wamekaa meza tofauti.

Aliongeza kuwa inadaiwa kuwa muda mfupi mumewe alionekana akiongea na kundi la wanaume, muda mfupi marehemu alienda kujisaidia ambapo hakurejea tena hadi mwili wake ulipokutwa umetelekezwa eneo
hilo.

Hata hivyo, imedaiwa kuwa kabla ya tukio hilo mumewe baada ya kuongea na kundi la wanaume alitoweka ghafla.

Kamanda Matei alisema baada ya taarifa hiyo polisi walifika na kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu uliokuwa mtupu na kubaini kuwa
sehemu zake za siri zilikuwa zimeingiliwa na kukuta mabaki ya mbegu za kiume.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya, Tengeru na Polisi wanamshikilia mume wa marehemu huyo kwa mahojiano zaidi huku watuhumiwa wengine wakiendelea kutafutwa.

No comments: