Wednesday, September 8, 2010

Warembo Miss Tanzania wanusurika kufa baharini!


Hemed Kisanda na Jelard Lucas wa GPL wanaripoti
WAKATI Watanzania wakiwa na hamu kubwa kutaka kumjua ni nani atatwaa Taji la Miss Tanzania mwaka huu, ni Mungu tu ndiye aliyeweza kuokoa maisha ya warembo hao kufuatia kupinduka kwa mtumbwi waliokuwa wamepanda kuelekea katika kisiwa kimoja ndani ya Bahari ya Hindi kwa ajili ya kupiga picha.


Hali hiyo ilitokea Jumapili iliyopita umbali wa mita 15 kutoka ufukwe wa Bahari ya Hindi karibu na Hoteli ya Giraffe, Mashariki mwa Jiji la Dar e Salaam ambako warembo hao wameweka kambi tayari kwa shindano hilo.

Imeelezwa kwamba tukio hilo ambalo lingeweza kupoteza uhai wa warembo hao lilitokea baada ya mtumbwi huo kukumbwa na dhoruba kufuatia kuchafuka kwa hali ya hewa baharini.


Lundenga akipiga mbizi
Kwa mujibu wa habari tulizozipata, ndani ya mtumbwi huo kulikuwa na warembo tisa ambao walikuwa wakitangulia kwenda katika kisiwa hicho kabla ya mtumbwi huo kurudi kuwachukua wengine.

Risasi Jumatano limeweza kupata majina ya warembo waliokuwa katika mtumbwi huo kuwa ni Angelina Ndege (Lindi), Salma Mwakaluka (Dar City Centre), Flora Martin (IFM-Vyuo Vikuu), Fatma Ibrahim (Kanda ya Ziwa- Mara), Magreath Godson ( Kanda ya Ziwa- Shinyanga) , Shadya, Christina Justine (Chuo Kikuu Huria) na Ummy Malik (Sinza- Kinondoni) na mmoja ambaye jina lake halijapatikana.


Dalili za kutokea kwa ajali hiyo zilianza kuonekana mita 10 baada ya mtumbwi huo kuanza safari ambapo ulipofika mita 15 kutoka nchi kavu hali ya hewa ilibadilika na mawimbi mazito yakaanza kuupiga hivyo kushindwa kuhimili kasi na kupinduka.

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko muda mfupi baada ya taarifa hizo kutolewa, Mkurugenzi wa Kamati ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga ‘Anko Hashimu’ alikiri kutokea kwa ajali hiyo na kusema ilikuwa ya kawaida kama ambavyo ajali nyingine zinavyotokea.



“Ni kweli ajali imetokea lakini ni ya kawaida kama zinavyotokea ajali nyingine,” alisema Lundenga na kuongeza kuwa, walifahamu kwamba warembo wengi hawajui kuogelea hivyo walijiandaa kwa kuwapa majaketi maalum ya kuogelea ‘Life-jackets’.

“Kama vile haitoshi, tulishaandaa boti yenye kasi ‘speedboat’ kwa ajili kutoa msaada kwa lolote ambalo lingeweza kutokea,” alisema Lundenga.

Katika hatua nyingine, Lundenga amewashukuru wazazi wa walimbwende hao kwa kuwa na moyo wa uvumilivu hata baada ya taarifa za tukio hilo kutolewa.

“Kwa kweli tunashukuru kwa uvumilivu wao maana kama wangekuwa na moto ingekuwa balaa,” alisema Lundenga.

Aidha, aliongeza kwamba, warembo wote walipatiwa matibabu maalum ya kuwarudisha katika hali zao za kawaida na wako tayari kwa ajili ya shindano.

Katika hatua nyingine mmoja wa warembo walio katika kinyang’anyiro hicho (jina tunalo) ameliambia gazeti hili kuwa kulizuka hofu kubwa na vilio kutawala baada ya hali ya hewa kuchafuka na hatimaye kupinduka kwa mtumbwi na kuwaacha wakizama baharini kabla ya kuokolewa na waogeleaji waliokuwa kwenye ‘Speedboat’.

No comments: