Tuesday, September 14, 2010

Askari Usalama wa Taifa ajimiminia risasi mdomoni, afa

OFISA wa Usalama wa Taifa , Bw. Mzee Mnyete (32), amejiua kwa kujipiga risasi mdomoni iliyotokea kichwani na maiti yake imekutwa ikiwa imelala kitandani chumbani kwake ghorofa ya nne Block 'A' Makumbusho Kijitonyama kwenye nyumba za Usalama wa Taifa.


Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari maiti hiyo iligundulika jana saa 2:45 asubuhi wakati ofisa huyo akitafutwa kwa ajili ya kazi maalum na viongozi wake.

Ilidaiwa kuwa, baada ya ofisa huyo ambaye alikuwa hajaoa kutoonekana kazini jana, ndipo wenzake waliamua kwenda kwake na kukutwa mlango ukiwa umefungwa.

Baada ya kuchungulia kwa ndani waliona mwili wa ofisa huyo ukiwa umelala kitandani kwake, walipovunja mlango walibaini akiwa amekufa huku akiwa na jeraha la risasi mdomoni na kichwani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Bw.Elias Kalinga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ingawa alieleza kuwa alikuwa nje ya ofisi kutokana na kutojisikia vizuri.

" Nipo hospitali afya yangu si njema naumwa lakini hata mimi nimezipata taarifa hizi hivyo nitazifanyia uchunguzi wa kina,"alisema Kamanda Kalinga.

No comments: