Wednesday, March 9, 2011

Mwanaume muuaji wanawake aibuka Dar

Hali ya hatari imejitokeza hivi karibuni jijini Dar es Salaam baada ya kuibuka mwanaume mmoja anayedaiwa kuua wanawake.

Mwanaume huyo ambaye anasakwa na polisi, anadaiwa kuwa ndiye aliyewaua wanawake watatu kwenye nyumba za kulala wageni huku mwanamke mmoja akinusurika kufa.

Vifo hivyo vya kusikitisha vilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo Jumatano ya Februari 23, mwaka huu, aliyekuwa anadaiwa kuwa ni mwanafunzi wa Ubungo Islamic High School, Amina Ramadhani aliingia na mwanaume anayetuhumiwa kwa mauaji hayo kwenye nyumba ya kulala wageni iitwayo Mkomboni iliyopo Kinondoni Mkwajuni.

Baada ya muda mfupi mwanaume huyo aliondoka. Wahudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni (gesti) walimkuta msichana huyo kwenye chumba namba sita akiwa amekufa huku akichuruzika damu mdomoni.

Wakati mwili wa marehemu ukichukuliwa kwenye gesti hiyo, wahudumu na baadhi ya watu walidai kumwona mwanaume anayetuhumiwa kwa mauaji hayo kabla ya tukio hilo. Waliuelezea mwonekano wake kuwa ni mwembamba, mrefu, mweusi na anapenda kuvaa kofia ya kufunika uso ‘kapelo’. Walieleza kuwa haikuwa siku yake ya kwanza kulala kwenye gesti hiyo.

Mwili wa marehemu Amina ulitambuliwa na ndugu zake katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar, Februari 26, mwaka huu ambapo waliuchukua kwa ajili ya kwenda kuuzika.

Wakati Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni likijipanga kumsaka muuaji huyo, kesho yake mwanamke mwingine alikutwa amekufa kwenye gesti nyingine.

Mwanamke huyo ambaye mpaka jana Jumatatu mwili wake ulikuwa bado haujatambulika ukiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Temeke, alikutwa amekufa kwenye chumba namba 108 ndani ya ‘gesti’ ya Four A iliyopo Tandika Transformer jijini Dar.

Inadaiwa kuwa marehemu huyo naye aliingia chumbani na mwanaume aliyekuwa amevaa ‘kapelo’ anayeshukiwa kuwa ndiye aliyefanya mauaji ya awali.

Baada ya mwili huo kufanyiwa uchunguzi wa awali eneo la tukio, ulikutwa umekatwa sehemu za siri huku ukivuja damu nyingi puani, hali iliyoonesha kuwa kulikuwa na imani za kishirikina katika tukio hilo.

Inaelezwa kuwa baada ya kifo cha mwanamke huyo, mtuhumiwa alitokomea kusikojulikana ambapo Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke kwa kushirikiana na wenzao wa sehemu mbalimbali wanaendelea na juhudi za kumsaka mtuhumiwa.

Katika tukio hilo, wakazi walioshuhudia marehemu akitolewa kwenye gesti hiyo walionekana kuchanganyikiwa na kukumbushia tukio lingine la mauaji lililotokea hivi karibuni.

Katika tukio hilo, mwanamke mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Hadija ambaye aliingia kwenye nyumba ya kulala wageni ya Ngekewa akiwa na mwanaume mweye wajihi kama wa yule anayevaa ‘kapelo’ na baada ya muda mfupi akakutwa amefia chumbani katika mazingira ya kutatanisha.

Mwili wa Hadija ulikutwa umelala kitandani kwenye chumba namba sita cha ‘gesti’ hiyo huku mwanaume aliyeingia naye ambaye anatuhumiwa kwa mauaji hayo akitokomea kusikojulikana.

Baadhi ya watu waliowaona wauaji kabla ya matukio hayo wameeleza kuwa watuhumiwa hao wanaonekana katika mwonekano unaofanana na wengine kudai huenda ni mtu mmoja.

Inaelezwa kuwa mwanamke aliyenusurika kufa baada ya kutoka mbio chumbani akiwa na kanga moja, aliwaambia wahudumu wa nyumba moja ya kulala wageni ya Mkomboni iliyopo Kinondoni Mkwajuni, Dar kuwa alichokiona chumbani humo hajawahi kukiona maishani mwake.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi Temeke, David Misime, amewaomba wananchi kutulia wakati wakiendelea na uchunguzi na ametoa wito kwa mtu yeyote aliyepotelewa na ndugu yake ambaye ni mwanamke afike Hospitali ya Temeke kuutambua mwili wa mwanamke huyo

No comments: