Siku za hivi karibuni pamekuwa na minong'ono kwamba kuna mcheza mpira mmoja pale Uingereza anasadikika kuibanjua amri ya sita na mmoja wa aliyekuwa mshiriki katika kipindi cha televisheni cha Big Brother, Imogen Thomas.
Haraka haraka pakapitishwa sheria ya kulinda jina la mchezaji huyo wa mpira kutotolewa hadharani kwa sababu wanazozifahamu wao wenyewe. Leo, ghafla bin vuu, mbunge kwa tiketi ya chama cha Demokrasia ya Kiliberali, John Hemming, akatelezesha ulimi na kumtaja mchezaji huyo anayelindwa na sheria hiyo kuwa ni Ryan Giggs wa Man United. Bwana Hemming amekuwa mmoja wa wanaharakati ambaye amekuwa akipinga kwa mchezaji huyu kulindwa na sheria hiyo.
Sheria hii ilipitishwa mahsusi kuwabana watumiaji wa mtandao wa Twitter ambao walikuwa wameshalinyaka jina hilo na kuanza kumegeana ndogo ndogo kwa kasi ya sawa na moto wa nyika kwenye nyasi kavu. Hemming alipopewa nafasi ya kuuliza swali juu ya sheria hiyo, anayoamini imetungwa mahususi kuwafunga mdomo raia karibu 75,000 waliotumia Twitter kuhabarishana habari hiyo, alisema hakuna maana kuendelea kumlinda mchezaji huyo maadam jina lake limeshavuja kwa raia wa Twitter.
Akitumia nafasi ya kipekee katika ukumbi wa bunge, na bila shaka kujilinda kwa kanuni za bunge hilohilo, Hemming akajikuta akilianika jina Giggs dakika chache baada ya Mahakama Kuu ya Uingereza kutupilia mbali kesi iliyokuwa ikitaka sheria hiyo iliyokuwa mahsusi kumlinda Giggs ifutwe.
Hazikupita sekunde kadhaa kabla ya Hemming kuvutwa shati na spika wa Bunge hilo la Uingereza, John Bercow, ambaye ni spika kupitia chama cha Kihafidhina (Conservative). Bercow alisema, "Nafasi kama hii tuliyompa mbunge ni ya kujadili uhalali wa sheria hii na si kusimama na kusema chochote tu. Iwapo mbunge anataka kuendelea na hoja yake ya msingi na aendelee."
Duh! Unadhani ni kwa nini tumekuwa na mfululizo wa kesi za masuala ya uzinzi kwa watu maarufu, kwa kiasi kikubwa siku za hivi karibuni?
No comments:
Post a Comment