Tuesday, March 8, 2011

Babu wa Loliondo aiangukia Serikali

Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Ambilikile Masapila (kushoto) akiwa na msaidizi wake.

WAKATI idadi ya watu ikizidi kumiminika katika Kijiji cha Samunge, Tarafa Sale, Loliondo kupata kile kinachoaminika kuwa ni tiba dhidi ya magonjwa sugu, mtoa huduma hiyo, Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Ambilikile Masapila ameiomba Serikali imsaidie kupata gari la kubeba dawa, vyombo vya kunywea, kuni na vyombo vikubwa vya kuchemshia dawa hiyo ili kukabili wingi huo.

Mchungaji Masapila ambaye alistaafu utumishi wa Kanisa mwaka 2001, katika Usharika wa Sonjo, alisema licha ya dawa hiyo kutolewa kwa Sh 500, pia kuna tatizo kubwa la barabara hadi kufika kijijini hapo.

"Tunaomba Serikali kutengeneza barabara kwani wagonjwa wanapata shida sana kufika hapa, nasikia hata nauli zimepanda sana," alisema Masapila.

Gharama za magari zimeendelea kuwa juu kwani hivi sasa wale wanaokwenda kwa kutumia magari ya kitalii wanalazimika kulipa kati ya Sh120,000 na 150,000 na mabasi ni kati ya Sh30,000 hadi 50,000.

Magari hayo sasa yamekuwa yakiondoka Arusha usiku ili kufika Samunge usiku wa manane na hatimaye siku inayofuata wagonjwa wapate dawa.

Kuongezeka kwa kasi kwa watu wanaokwenda kutibiwa kwa mchungaji huyo kumeibua hofu ya kutokea kwa magonjwa ya milipuko kama kipindupindu na kuhara kutokana na kukosekana kwa huduma muhimu za kijamii.

Eneo hilo hivi sasa linakabiliwa na tatizo kubwa la huduma muhimu kama vile majisafi, vyoo, nyumba za kulala na vyakula hivyo wageni hao wengi wakiwa wanakabiliwa na maradhi sugu yakiwemo kansa, kisukari, shinikizo la damu, kifua kikuu na Ukimwi.

Akizungumza na Mwananchi jana, Msaidizi wa Mchungaji huyo, Paulo Dudui alisema maafa makubwa yakiwamo magonjwa ya mlipuko yanaweza kutokea kwa sasa... "Tunaomba (Serikali) msaada wa mahema, vyoo vya muda na huduma muhimu kama mawasiliano kwani hapa kuna watu zaidi ya 6,000 ambao wanalala nje hawana sehemu za kujisaidia, vyakula hakuna na hata mawasiliano hakuna."

Alisema gharama za maisha katika eneo hilo zimepanda kwani bei za vyakula hivi sasa ni kubwa mno akisema hali hiyo ni hatari hasa kwa wagonjwa wanaotolewa hospitali ambao hali zao zinaweza kuwa mbaya hata kabla ya matibabu na hivyo kufariki.

Alisema juzi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali aliwatembelea na kujionea hali hiyo na hivyo wana imani suala la msaada litafikishwa katika ngazi za juu.

"Hali ni mbaya sana hapa kama mvua zikinyesha zaidi kunaweza hata kutokea vifo kwani wengi wanaokuja hapa ni wagonjwa," alisema Dudui.

Kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa kunatokana na kusambaa kwa taarifa za watu waliopata tiba hiyo na kupona maradhi hayo sugu. Kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM Mkoa wa Arusha ambaye hakutaka kutaja jina lake alidai kuwa tangu alipokunywa dawa hiyo, tatizo la sukari ambalo lilikuwa likimsumbua limekwisha.

"Sijui kama nimepona kabisa au la, lakini sasa najisikia vizuri tofauti na mwanzo," alisema kiongozi huyo.

Diwani waViti Maalum (CCM) Wilaya ya Monduli, Dora Kipuyo alidai anamfahamu mgonjwa aliyekuwa na kansa ya mguu ambao ulitakiwa kukatwa, lakini baada ya kupata dawa hiyo sasa vidonda vimekauka.

Baadhi ya watu wenye Virusi Vya Ukimwi (VVU), ambao wamepewa dawa hiyo, licha ya kudai kuwa sasa wana hali nzuri, bado hawajapima kwani wengi waliohojiwa walikuwa hawajatimiza sharti la kukaa siku saba kabla ya kupima ili wajue kama virusi vimekwisha au la.

Mchungaji Masapila alisema dawa hiyo ambayo alioteshwa na Mungu tangu mwaka 1991 na kukumbushwa mwaka 2009, inatokana na maombi na mti wa mgariga ambao unapatikana katika viunga vya Milima ya Sonjo.

Hata hivyo, alisema kupona kwa mgonjwa haraka pia kutokana na imani yake juu ya dawa hiyo ambayo dozi yake ni kikombe kimoja tu kinachonywewa hapo hapo inakotolewa.

Tayari Wizara ya Afya, imekwishatuma wataalam wake kwenda huko kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa dawa hiyo.


CHANZO: MWANANCHI MACHI 08, 2011

No comments: