Monday, March 7, 2011

Watu wajazana Loliondo kupata Dawa

Juu na Chini msururu wa magari na watu kuelekea
Loliondo kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapile kupata tiba ya jero

MAELFU ya watu, wakiwemo vigogo wa serikali, wabunge na wafanyabiashara wakubwa nchini, wamefurika katika Kijiji cha Samunge Tarafa ya Sale wilayani Ngorongoro kupata 'dawa ya maajabu ya Mungu' inayodaiwa kutibu magonjwa mengi sugu ikiwamo Ukimwi.

Helkopta za wafanyabiashara na magari zaidi ya 1,000 yakiwamo magari ya serikali, binafsi na mashirika ya kimataifa ikiwamo Umoja wa Mataifa (UN) na Jumuiya ya Afrika Mashariki, yamefurika katika kijiji hicho kilichopo umbali ya takriban kilometa 400 kutoka Jiji la Arusha.
Wakubwa wakijisogeza Loliondo
Dawa hiyo, inatolewa na Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapile (76), ambaye anasema alioteshwa na Mungu kuitumia kutibu tangu mwaka 1991.

Mchungaji Mwasapile ambaye alifanya mahojiano na Mwananchi Jumapili nyumbani kwake wakati akiendendelea kutoa dawa kwa wagonjwa wake, anasema ndoto hiyo aliendelea kuota mara kadhaa hadi Agosti 26 mwaka jana alipoanza rasmi kutibu.
Mchungaji Mwasapile akihojiwa na waandishi

Anasema dawa hiyo inatokana na mti aina ya mugariga na yeye pekee ndiye anaweza kukupatia na kunywa kikombe kimoja pekee na ukinywa tu inaanza kazi ya kutibu maradhi sugu ya ukimwi, kisukari, pumu na saratani.
Wananchi wakikinga vikombe kupatiwa dawa na
Mchungaji Ambilikile Mwasapile kwa bei ya sh. 500 tu

Mchungaji Mwasapile anasema gharama za dawa hiyo ni Sh500 tu na dozi yake ni kikombe kimoja tu na hairuhusiwi kurudia kuinywa. Kabla ya kukamilika mchungaji huyo huiombea dawa hiyo na kuichemsha katika maji safi.

“Mungu ameniotesha kutoa dawa hii kwa Sh 500 aliponiambia hata mimi nilishangaa. Kwanza aliniambia niwape watu wapone saratani, kisukari, pumu na magonjwa mengine na baadaye akanionyesha kuwa dawa hii niwape hata wagonjwa wa ukimwi na watapona,“ anasema Mwasapile.

Habari hii imeandikwa Mussa Juma
na Daniel Sabuni, Loliondo.
Picha zote kwa hisani ya Aman Masue.

No comments: