Monday, April 23, 2012

HOJA YA KUTOKUWA NA IMANI NA WAZIRI MKUU BUNGENI KWA MUJIBU WA KATIBA IBARA YA 53A NA KANUNI YA BUNGE, KIFUNGU CHA 133 KUWASILISHWA KWA SPIKA LEO

HOJA YA KUTOKUWA NA IMANI NA WAZIRI MKUU BUNGENI KWA MUJIBU WA KATIBA IBARA YA 53A NA KANUNI YA BUNGE, KIFUNGU CHA 133 KUWASILISHWA KWA SPIKA LEO


Masharti yametimizwa; wabunge 73 wazalendo wamesaini
Ni mwendelezo wa ‘operesheni uwajibikaji’
Mnamo tarehe 19/04/2012 wakati nahitimisha hoja ya Kamati ya Mashirika ya Umma nilieleza kusudio langu la kuwaomba waheshimiwa wabunge waniunge mkono katika kutia saini zisizopungua asilimia 20 ya wabunge wote ili kuweza kutimiza matakwa ya Katiba ibara ya 53A kwa ajili ya kuwasilisha Bungeni hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.Mnamo tarehe 20/04/2012 niliandaa orodha ya waheshimiwa wabunge wote na kuisambaza ndani na nje ya ukumbi wa Bunge ili waheshimiwa wabunge wote waweze kutia saini hizo, na mpaka leo tarehe 22/04/2012 orodha hiyo imetimiza idadi ya wabunge wazalendo wanaopigania uwajibikaji 73 kutoka vyama vyote vyenye uwakilishi Bungeni, isipokuwa chama cha UDP ambacho kina Mbunge 1 na hajatia saini waraka huo mpaka sasa.

Kwa mujibu wa kanuni za Bunge kifungu cha 133 (1) kinasomeka “Mbunge yeyote anaweza kutoa taarifa ya maandishi kwa Spika ya kutaka kuleta hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu kwa mujibu wa ibara ya 53A ya Katiba” na kwa mujibu wa kifungu kidogo cha (3) kinasomeka “hoja ya kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu haitajadiliwa na Bunge isipokuwa tu kama;

“taarifa ya maandishi iliyowekwa saini na kuungwa mkono na Wabunge wasiopungua asilimia 20 ya wabunge wote itatolewa kwa Spika, siku zisizopungua kumi na nne kabla ya siku inayokusudiwa kuwasilishwa Bungeni;”

Hali kadhalika kanuni za Bunge Kifungu cha 133 (4) kinasomeka kuwa “hoja inayotolewa chini ya Kanuni hii na iliyotimiza masharti ya Katiba,itawasilishwa Bungeni mapema iwezekanavyo na itaamuliwa kwa kura za siri”.

Hivyo basi baada ya kutimiza matakwa ya kikatiba na kanuni za Bunge leo tarehe 23/04/2012 nitawasilisha rasmi kwa Spika Taarifa ya Maandishi kwa mujibu wa kanuni 133 (1) na (3) ya hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu kwa kushindwa kusimamia uwajibikaji wa Serikali bungeni kwa mujibu wa ibara ya 52 na hivyo kulinda mawaziri wenye kusababisha matumizi mabaya ya fedha za umma na kulisababishia hasara taifa.

Tunatarajia kwamba siku kumi na nne baada ya kuwasilisha hoja hiyo bunge litakutana kwa haraka kujadili hoja hiyo ili kuwezesha uwajibikaji na hatua kuchukuliwa za kuhakikisha mapendekezo ya ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na maazimio ya Bunge yanatekelezwa. Hoja hii ni mwendelezo wa ‘operesheni uwajibikaji’ hivyo tunaomba wabunge na watanzania wote waiunge mkono ili kunusuru uchumi wa nchi na kuchangia katika ustawi wa wananchi.

Kwa niaba ya wabunge waliotia saini kuunga mkono taarifa ya hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu;

…………………………….

Kabwe Zuber Zitto.Mbunge Jimbo la Kigoma Kaskazini.

22/04/2012.


No comments: