
KAMA wewe ni kijana mdogo na ndio kwanza umeajiriwa, kwa vyovyote vile utapata ugumu unapotaka kujenga jina lako kazini kwako na kutambuliwa kwa mchango wako. Pengine
changamoto kubwa ni kujitambulisha bila kuonekana kama vile unajidai au una mmajvuno.
Iwapo mara kwa mara utasikika ukijisema jinsi ulivyo maridadi, jinsi unavyoiweza kazi yako na jinsi shirika au kampuni yako ilivyo na bahati kwa kuwa na wewe
utachukuliwa kuwa mtu wa majigambo na kujiinua. Namna hii utapuuzwa.
Lakini pia ukikaa kimya kabisa unaweza kujikosesha fursa ya kupewa majukumu fulani ya kukujengea jina. Hushauriwi kujipigia debe kwa maneno na kwa kujipendekeza kwa
mabosi, lakini angalau uchukue jitihada za kuwaonesha watu wanaokuzunguka kuwa unao mchango muhimu katika eneo lako la kazi. Zipo mbinu ambazo ukizitumia vema zitakusaidia.
Fahamu lengo lako
Kabla ya kuanza kujipigia tarumbeta na kuimba sifa zako mwenyewe kazini, jiulize lengo lako la kufanya kazi kwa bidii ni nini hasa. Je, kuna mtu unataka kuchukua nafasi yake? Je, unataka mtu fulani akuone unavyowajibika? Je, unataka kuwafurahisha wakubwa wa kampuni?
Kama hujui hatimaye unataka jitihada zako zikufikishe wapi, haitakuwa rahisi kufahamu kama uko katika njia sahihi au kama umefika. Lakini ili ufanikiwe, hakikisha kuwa lengo lako la kujiboresha linakwenda sanjari na malengo ya shirika
lako, pamoja na malengo maalumu ya idara au kitengo chako.
Hakikisha una mafanikio yanayopimika
Ili uweze kuwa na ujasiri wa kujisifia – kama ni lazima kufanya hivyo – hakikisha kwanza unalo jambo la kujisifia kwalo, maana huwezi kujisifu bila sababu. Hakikisha unacho kitu maalumu ulichofanikiwa kukifanya na kiwe kinapimika.
Katika kazi, kama kitu unachokiita mafanikio huwezi kukipima basi hoji uhalali wa kukiita kitu hicho mafanikio. Kadiri itakavyowezekana, hakikisha unapojisifia uwe na jambo maalumu ambalo mtu akikuuliza unajisifu kwa lipi uweze kumwonesha, na liwe linapimika.
Lenga zaidi mambo makubwa
Unapokuwa na mawazo mafupi utajikita zaidi katika mambo madogo madogo. Kama utakuwa mtu wa kujitapa kwa mambo madogo madogo utakuwa kichekesho na kila mmoja atajua
unayoyaweza ni hayo madogo. Zaidi ya hapo, hakuna mtu atakayeona jipya kwako.
Mafanikio madogo yaweke moyoni mwako – watu watayaona tu hata usiposema. Badala yake, weka msisitizo katika mambo makubwa, mathalani mambo ambayo kila mtu anayafikiria na yanamtia hofu. Kuna jambo ambalo ukilifanya kila mtu atakuona shujaa, jitahidi kulifanya hilo.
Sifa zako zifanye za kampuni
Unapofanikisha jambo, lazima tu utajisikia vema na unaweza hata kujivuna. Hata hivyo, iwapo utajaribu kuonesha kuwa mafanikio ya kampuni/shirika umeyaleta wewe utalitia tembo maji, maana watu wengine wote hawatakuunga mkono, kwani yamkini nao watajiona wanafanya kazi, si kucheza.
Kwa hiyo, badala ya kutembea ukijitangaza kuwa wewe ndiwe kinara wa kampuni/shirika, ashiria tu kwamba mafanikio yaliyopatikana ni ya shirika zima na yameletwa kwa
ushirikiano wa wadau wote.
Kwa kufanya hivi, mbali na kwamba watu watatambua kuwa ni wewe uliyefanikisha jambo husika, lakini pia watakuona jinsi ulivyo muungwana kwa kutopenda kujisifia.
Usikubali kukatishwa tamaa
Kuna wakati ambapo utajiona kana kwamba huna maana, mathalani bosi wako anapokupuuza au kukataa pendekezo lako. Lakini wakati mwingine bosi wako anaweza kuwa tu ametingwa na hakumaanisha kukupuuza.
Kumbuka hata kama bosi wako ni mkubwa kiasi gani na yeye anao watu anaowajibika kwao, huku pia akiwa na kazi zake, halafu pia akitakiwa kukusikiliza wewe na wengine
walio chini yake. Siku moja ukifika ngazi ya menejimenti utaelewa.
Kwa hiyo, usijisikie vibaya iwapo bosi ataonekana kutokusikiliza vizuri. Badala ya kuvunjika moyo, endelea kushirikiana na bosi wako na hakika mchango wako utabainika siku muafaka ikifika.
Watu husema raha mtu hujipa mwenyewe. Kazini kwako wewe ndiwe mtu wa kwanza kujitakia heri na mafanikio na kwa hiyo lazima ufanye jitihada za kulitangaza jina lako kwa mustakabali mwema wa maisha yako. Isipokuwa tu utapaswa kuwa makini, maana ukijiinua mwenyewe utashushwa.
Isipokuwa tu kwa kuendelea kuwa mwaminifu kwa wakubwa
zako, huku ukiyachukulia mafanikio yako kuwa mafanikio ya kampuni, utaonekana na kutambuliwa zaidi.
No comments:
Post a Comment