Tuesday, December 8, 2009

Mtuhumiwa mauaji abambwa kavaa baibui

Na Suleiman Abeid, Shinyanga

MWANAFUNZI mmoja wa Shule ya Sekondari anayetuhumiwa kufanya mauaji mkoani Mwanza na kutorokea Shinyanga
amekamatwa na akiwa amevaa mavazi ya kike aina ya baibui akiwa katika harakati za kutoroka.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Daudi Siasi amemtaja mwanafunzi aliyekamatwa kuwa ni Daudi Rashidi (18) ambaye pia hutumia jina la Athumani Rashidi
anayetuhumiwa kumuua mwanafunzi mwenzake jijini Mwanza wiki iliyopita.

Kamanda Siasi alisema mbali ya mwanafunzi huyo ambaye alikamatwa juzi katika kituo kikuu cha mabasi mjini Shinyanga, polisi iliwakamata watu wengine watatu
wanaodaiwa kushiriki katika mauaji hayo.

Wengine waliokamatwa ni Nixon Robert (18), pia mwanafunzi wa sekondari anayetuhumiwa kushiriki kumpiga mwanafunzi aliyekufa, Bw. Ally Rashid (40) mfanyabiashara wa Mtaa wa Rufiji mjini Mwanza ambaye anadaiwa kuwatorosha wanafunzi hao na Bi. Margaret George (25) mkazi wa Ndembezi, Shinyanga aliyekuwa awapatie hifadhi.

Mtuhumiwa Daudi alishtukiwa na abiria wenzake aliokuwa nao katika basi hilo kutokana na sauti yake kuwa ya kiume
wakati mavazi aliyokuwa amevaa ni ya kike ikiwa ni baibui nyeusi iliyokuwa imeficha uso wake wote na kuachia uwazi kidogo katika sehemu ya macho na hivyo kutoa taarifa polisi.

"Baada ya kuwakamata tuliwasiliana na wenzetu wa Mwanza ambao baada ya kuwatajia majina ya Daud na Nixon waliwatambua kuwa ndiyo wanaowatafuta kuhusiana na kesi ya
mwanafunzi wa sekondari aliyeuawa kwa kipigo na sasa
tunaandaa mipango ili kuwarejesha Mwanza kujibu shtaka la mauaji," alieleza Kamanda Siasi.

Hata hivyo, Kamanda huyo alisema kuwa polisi walikuwa na taarifa za siri zilizotolewa na raia wema mkoani Mwanza, kwamba wanafunzi hao na mtu anayewasaidia kuwaficha wametorokea Shinyanga.

Kutokana na taarifa hizo na raia walimshtukia mmoja wa watuhumiwa polisi walifanikiwa kuwanasa wakati wakiteremka kwenye basi la Kampuni ya Mohamed Trans mjini Shinyanga.

No comments: