Timu ya Ijumaa, Dar na Morogoro
Ikiwa ni siku nne tu tangu ulipotokea msiba mkubwa wa wanamuziki 13 wa Bendi ya Taarab ya Five Stars ya jijini Dar es Salaam, nyuma ya tukio hilo yameibuka mambo mazito ya kusikitisisha, Ijumaa lina ‘pakeji’ kamili.
Katika tukio hilo baya, wanamuziki hao wakiwa ndani ya gari aina ya Toyota Coaster lenye namba za usajili T 351 BGE, Machi 21, mwaka huu saa tatu usiku wakitokea Kyela, Mbeya, walipofika eneo la Mikumi, Morogoro, gari lao lililivaa lori aina ya Fuso lililokuwa limebeba mbao na kusababisha vifo hivyo papo hapo.
Wanamuziki waliopoteza maisha eneo la tukio ni pamoja na Issa Hassan ‘Kijoti’ (M’chumu), Husna Mapande, Sheba Juma, Omary Hashim, Hamisa Mussa, Ramadhan Maheza’Kinyoya’, Omary ‘Tall’, Hajji Mdahaniwa, Samir Maulid, Hassan Ngereza, Maimuna Makuka ‘Kisosi’ wa Kundi la Kitu Tigo, Hajji Babu na Tizo Mgunda.
Walionusurika ni Ali Juma ‘Ali J’, Mwanahawa Ali, Suzane Benedict, Rajab Juma, Issa Kamongo, Mwanahawa, Mifupa na Hammer Q.
Nyuma ya vifo hivyo inaelezwa kwamba kuna mambo mengi yaliyogubika tukio hilo kama ifuatavyo;
SIRI YA AJALI YAFICHUKA
Kwa mujibu wa mashuhuda waliofika eneo la ajali muda mfupi baada ya tukio hilo, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa Coaster ambaye hakuwa makini katika kulipita lori lililoegeshwa pembeni likiwa na viashiria vyote vya barabani.
Ilidaiwa kwamba, wakati anataka ‘kuliovateki’ lori hilo lililojaza mbao, ndipo alipokutana uso kwa uso na gari lingine aina ya Toyota Canter lakini katika jitihada za dereva kurudi upande wake ndipo akalivaa lori hilo.
WALITABIRI VIFO VYAO
Katika hali ya kushangaza, Ijumaa limemwagiwa data kuwa, baadhi ya wanamuziki waliopoteza maisha walitabiri vifo vyao.
Ishara hizo walizozionesha wanamuziki hao siku chache kabla ya tukio hilo, ziliwekwa kweupe na ndugu zao katika mahojiano maalum na waandishi wetu kwenye Ukumbi wa Equator Grill, Temeke Dar unaotumiwa na kundi hilo siku ya Jumanne Machi 22, mwaka huu wakati wa kuaga miili ya marehemu.
Waliopata nafasi ya kueleza kauli za mwisho za marehemu hao ni pamoja na ndugu wa Issa Kijoti, Tizo Mgunda, Hamisa Musa, Maimuna Makuka na Husna Mapande.
Akizungumzia kauli ya mwisho aliyoitoa Issa Kijoti kabla ya kwenda safarini Kyela, Mbeya, shangazi wa mwanamuziki huyo ambaye hakupenda jina lake lichorwe gazetini alikuwa na haya ya kusema:
“Nakumbuka kabla ya kusafiri alimfuata mama yake akamuomba amuoshe miguu kwa sababu alikuwa anakwenda safari ya mbali.
“Alimwambia ‘Mama, safari ninayokwenda ni ya mbali sana na bado mimi ni mtoto wako.’”
Aidha, shangazi huyo aliongeza kuwa, baada ya Kijoti kutoa ombi hilo, mama yake alimuosha miguu na kumpa baraka ndipo akaondoka na hakufanikiwa kurudi akiwa hai.
Kwa upande wake jirani wa marehemu Tizo aliyetambulisha kwa jina la Ashura Abdallah alisema: “Siku alipokuwa anasafiri aliniambia hakujisikia kabisa kusafiri lakini alilazimika kufanya hivyo kwa sababu ilikuwa safari ya kikazi.”
“Roho yake ilikuwa nzito sana, alihisi safari ingekuwa mbaya.”
Kwa upande wake rafiki wa karibu wa marehemu Hamisa Mipango aliyejitambulisha kwa jina moja la Ashura alisema: “Nakumbuka Hamisa hakuwa amejipanga vizuri kwa ajili ya safari, alikuwa anasitasita.”
Naye jirani wa marehemu Husna Mapande alisema: “Siku ya safari alinifuata akaniaga kuwa anakwenda safari lakini katika mazungumzo yetu aliniambia alitamani sana kuvaa nguo mpya, alimwita mtoto wake mmoja na kumuaga kuwa anakwenda safari.”
Baba mzazi wa marehemu Maimuna Makuka, mzee Bakari Mohamed akielezea kauli ya mwisho ya binti yake mara tu baada ya kupata ajali, alikuwa na haya ya kusema:
“Maimuna alinipigia simu wakati anapelekwa hospitalini, alinieleza kuwa amepata ajali na wenzake. Aliniambia hakuwahi kukutana na tukio kama hilo hivyo alihisi anakufa, alipofikishwa hospitalini akafariki.”
Hadija Kopa naye chupu chupu
Malkia wa mipasho nchini, Khadija Omar Kopa amesema kuwa Mungu ndiye amemnusuru na ajali iliyoua wanamuziki 13 wa Kundi la Five Stars Modern Taarab, vinginevyo naye angekuwa marehemu.
Kopa aliliambia gazeti hili mapema wiki hii kuwa, alitakiwa kuwemo kwenye msafara wa kundi hilo kwenye ziara zake za Mikumi na Iringa lakini alitofautiana na mapromota kwa upande wa masilahi.
“Kimsingi tungekubaliana katika masilahi, bila shaka ningekuwemo kwenye ajali na leo hii pengine ningekuwa marehemu. Nawasikitikia ndugu zangu waliokufa, pia namshukuru Mungu kwa kuniepusha na ajali,” alisema Kopa.
Mzee Yusuf alilia bifu lake na Issa Kijoti
Mkurugezi wa Kundi la Jahazi Modern Taarab, Mzee Yusuf ‘Mfalme’ amesema kuwa kifo cha mwimbaji wa Kundi la Five Stars Modern Taarab, Issa Musa ‘Kijoti’, kinamuumiza moyo wake kwani kimetokea kabla hawajamaliza tofauti zao.
Mzee aliliambia Ijumaa katikati ya wiki hii kuwa, tangu Issa Kijoti ahame Jahazi na kujiunga na Five Stars hakuwahi kukutana naye wala kusalimiana naye kwa njia ya simu, hivyo inamuuma mno.
“Kifo hiki kinaniumiza sana kwani nahisi atakuwa amekufa na kinyongo lakini mimi nimemsamehe kwa yote yaliyotokea,” alisema Mzee huku akifuta machozi.
Isha Mashauzi, Hadija Yusuf wazimia
Waimbaji wa taarab kutoka Kundi la Jahazi Modern, Isha Ramadhan na Hadija Yusuf wamejikuta wakizimia kwa uchungu kufuatia kuondokewa na wenzao waliopata ajali ya gari siku ya Jumatatu wakiwa wanatoka Kyela Mbeya kwenda Dar es Salaam.
Waandishi wetu walifika katika maskani ya Kundi la Five Stars, Equator Grill, Temeke ambapo waombolezaji walikusanyika kwa lengo la kuwaaga marehemu na kushuhudia wasanii hao wakiwa katika hali hiyo.
Miili ya marehemu ilipowasili saa moja usiku, wasanii waliokuwepo walikatisha mazungumzo na kuanza kulia ambapo Isha alimwaga machozi huku akiwataja kwa majina marehemu.
Ghafla mwanadada huyo alipoteza fahamu na kutoa kibarua kizito kwa wenzake kumpepea kabla ya kurejea katika hali yake ya kawaida.
Wakati Isha akipewa huduma ya kwanza, Khadija Yusuf naye akijikuta akidondoka kwenye kiti kwa uchungu na kuzimia papo hapo ambapo kazi ya kumweka sawa ilikuwa kwa wifi yake, Leilah ambaye alikuwa karibu yake.
Waimbaji hao walipozinduka kwa wakati tofauti, walikuta baadhi ya miili ya marehemu imeshaondolewa kwa ajili ya mazishi yaliyofanyika usiku wa Jumanne.
No comments:
Post a Comment