Tuesday, January 17, 2012

PAPAI: KINGA YA UGONJWA WA MOYO, SARATANI NA MAGONJWA MENGINE



PAPAI, tunda lenye ladha nzuri kama sukari, siyo tu ni tamu kulila, lakini ni chanzo kikuu cha virutubisho vinavyotoa kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali ya mwili, yakiwemo yale hatari ambayo huchukua maisha ya watu kila kukicha. Leo soma faida za tunda hili ili ujiepushe na maradhi ambayo yangeweza kukusumbua.
Kinga dhidi ya magonjwa ya moyo
Utaona kwamba maradhi ya moyo yana kinga karibu katika kila tunda au chakula cha asili. Tumeona vyakula kama karanga, korosho, zinavyoweza kutoa kinga dhidi ya magonjwa ya moyo, tunaona papai nalo limo kwenye orodha ya vyakula vinavyotoa kinga ya ugonjwa huo.
Inaelezwa kuwa papai ni kinga ya ugonjwa wa moyo unaotokana na kuziba kwa mishipa ya damu (atherosclerosis ) na ule unaotokana na kupatwa na ugonjwa wa kisukari (diabetic heart disease). Kwa kula papai mara kwa mara unajiepusha na magonjwa hayo.

HURAHISISHA MFUMO WA USAGAJI CHAKULA
Papai pia limeonesha kuwa na uwezo mkubwa sana wa kutoa kinga dhidi ya ugonjwa wa saratani ya utumbo ambayo hutokana na mtu kuwa na matatizo katika mfumo wake wa usagaji chakula. Papai huboresha mfumo mzima wa usagaji chakula na kumfanya mtu kupata choo laini na hivyo kujiepusha na madhara ya kukosa choo kwa muda mrefu na hatari ya kupatwa na kansa ya tumbo.

KINGA DHIDI YA UVIMBE NA VIDONDA
Watu wanaosumbuliwa na majipu au kutokewa na uvimbe wa ajabu ajabu na kupatwa vidonda mara kwa mara, inatokana na kutokuwa na virutubisho muhimu ambavyo hupatikana kwenye tunda hili. Imegundulika kuwa watu wenye matatizo hayo wanapotumia papai au virutubisho vyake hupata nafuu haraka na kupona.

KINGA YA MWILI
VITAMIN C na Vitamin A inayopatikana mwilini kutokana kirutubisho aina ya ‘beta-carotene’ kilichomo kwenye papai, ni muhuimu sana kwa kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya magonjwa yanayojirudia mara kwa mara, kama vile mafua, kuumwa sikio, kikohozi, n.k

NURU YA MACHO
Kama karoti inavyoaminika katika kuimarisha nuru ya macho, papai nalo ni miongoni mwa matunda ya jamii hiyo. Imeelezwa kuwa watu wanaotumia tunda hili hujipa kinga madhubuti ya macho na pia kudhibiti kasi ya kuzeeka ambayo huendana na umri wa mtu.

TIBA YA MAPAFU
Kama wewe ni mvutaji sigara mzuri au mtu ambaye katika mazingira yako unayoishi, hukumbana na moshi wa sigara, basi utumiaji wa vyakula vyenye kiwango kikubwa cha vitamin A kama papai, kutakuepusha na madhara yatokanyo na moshi wa sigara.

SARATANI YA KIBOFU
Ulaji wa papai na chai ya kijani (green tea) kutakuepusha na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa saratani ya kibofu – utafiti wa hivi karibuni uliochapishwa na  Asia Pacific Journal of Clinical Nutrition, umeeleza. Kwa faida hizi na nyingine, tupende kula tunda hili ili tujiepushe na magonjwa hatari yanayosumbua watu kila siku.
Kumbuka kwamba, kabla mwili haujapata hitilafu yoyote ya kiafya, kila tunda asilia unaloweza kulila, lina faida kubwa mwilini na huwa ndiyo kinga madhubuti ya mwili dhidi ya maradhi mbalimbal
i

No comments: